Taarifa ya Kataib Hizbullah imetolewa baada ya shambulio la Jumatano iliyopita la kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) kwenye Haram ya mjukuu ya Mtume Muhammad (saw), Sayyid Ahmad bin Musa al Kadhim (Shah Cheragh) (as) katika mji wa Shiraz, makao makuu ya mkoa wa Fars, kusini mwa Iran, lililoua watu 15, wakiwemo watoto 2. Hujuma hiyo pia imejeruhi waumini wengine 30.
Hujuma hiyo ya kigaidi, ambayo Daesh imechukua jukumu la kuhusika nayo, imelaaniwa na Umoja wa Mataifa na nchi mbalimbali za dunia.
Katika taarifa yake, Kataib Hizbullah ya Iraq imelaani jinai ya kigaidi katika Haram tukufu ya Shah Cheragh huko Shiraz na kutangaza kuwa, Saudi Arabia inang'ang'ania harakati yake chafu na ya kichochezi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na inatumia vyombo vichafu vya habari katika lugha zote ili kuvuruga usalama na amani katika miji mbalimbali ya Iran na inatumia nyenzo zote kwa ajili ya kudhoofisha mfumo wa Kiislamu wa Iran.
Taarifa ya Kataib Hizbullah imeendelea kusema kuwa: "Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, hakuacha njia yake ya umwagaji damu na uadui na sasa amechochea tawi lake la siri la kutenda jinai na la kitakfiri, yaani kundi la kigaidi la Daesh, kufanya uhalifu wa kutisha dhidi ya raia na wanawake wasio na ulinzi, watoto na wazee na kulenga eneo takatifu la kidini katika mji wa Shiraz."
Taarifa hiyo inaongeza kuwa, hivi ndivyo Bin Salman anavyoendeleza uadui na chuki yake ya kikaumu kwa ajili ya kuwaridhisha mabwana zake wa Kiamerika na Kizayuni.
Harakati ya Kataib Hizbullah ya Iraq ameyataka mataifa yaliyoathiriwa na jinai za kitakfiri za Saudia hususan katika nchi za Iraq, Syria, Lebanon, Yemen, Iran, Bahrain na Libya, kung'oa pembe ya Shetani katika ardhi tukufu za Hijaz na kukomesha utawala wa nasaba iliyolaaniwa ambao umekuwa chombo kiovu kinachotumiwa kupiga vita Uislamu na Waislamu.
342/